Mkurugenzi wa Habari na Uenezi wa Chadema, John Mnyika PICHA|MAKTABA |
Dar es Salaam.Kamati Kuu ya Chama cha
Demokrasia na Maendeleo (Chadema), leo inaanza kikao chake cha siku
mbili ikitarajiwa kujadili masuala mazito, hasa misukosuko iliyokikumba
katika siku za karibuni.
Taarifa iliyotolewa jana na Mkurugenzi wa Habari
na Uenezi wa Chadema, John Mnyika ilisema kikao hicho kitakachofanyika
Dar es Salaam kitapokea, kujadili na kufanya uamuzi wa masuala
mbalimbali ikiwamo hali ya siasa na ripoti ya fedha.
“Suala mojawapo litakuwa kujadili mihutasari ya
mikutano iliyopita na yatokanayo na mikutano hiyo, taarifa ya hali ya
siasa na ripoti ya fedha,” ilisema taarifa hiyo ya Mnyika, ambaye yuko
ziara ya kikazi huko Uturuki.
Pia utajadili mchakato na maudhui ya mabadiliko ya
katiba, taarifa ya utekelezaji wa Programu ya Chadema ni Msingi na
shughuli za kanda na taarifa ya utekelezaji wa Mpango Mkakati kuhusu
maboresho.
Chadema katika mawimbi makali
Miongoni mwa mambo ambayo yanatarajiwa kujadiliwa
katika kikao hicho ni mustakabali wake katika kipindi hiki ambacho
kinapita katika mawimbi makali kutokana na kuibuka kwa malumbano ya
waziwazi baina ya viongozi wake waandamizi na pia kusimamishwa kwa
baadhi ya viongozi wa mikoani.
Matukio ya karibuni yanajumuisha malumbano kati ya
Naibu Katibu Mkuu, Zitto Kabwe na Mbunge wa Arusha Mjini, Godbless Lema
kuhusiana na masuala ya posho, kusimamishwa kwa Mwenyekiti wa Chadema
wa Mkoa wa Arusha, Samson Mwigamba, kuvunjwa kwa uongozi wa Mkoa wa Mara
na pia kuondolewa kikaoni kwa Mbunge wa Maswa Magharibi, John Shibuda.
Wafuatiliaji wa mambo ya siasa watakuwa
wanakitazama kikao hiki kama fursa ya kuweka sawa mambo ili kiendelee
kutoa ushindani kwa chama tawala.
Alipoulizwa kama matukio ya hivi karibuni
yatajadiliwa katika kikao hicho, Mnyika alikataa kuingia kwa undani na
badala yake alisema taarifa zitatolewa baada ya kikao.
“Niko nje ya nchi, mengine utapewa majibu kesho
(leo) kwa yale ambayo yatakuwepo katika taarifa zitakazowasilishwa. Yale
ambayo hayatakuwepo utajulishwa pia iwapo hayatajadiliwa,” alisema
Mnyika.
Zitto na Lema
Zitto na Lema waliingia katika vita ya maneno mwanzoni mwa Novemba kuhusiana na masuala ya posho ya vikao.
Vita hiyo ilianzishwa na Lema katika kikao cha wabunge wiki iliyopita aliposema kuwa Zitto anafanya unafiki kukataa posho.
Lema alimtuhumu Mbunge huyo wa Kigoma Kaskazini
kwamba anakataa posho za vikao bungeni, lakini anapokea posho nyingi
kutoka mashirika mbalimbali ya kijamii nchini.
Lema aliweka tuhuma hizo kwenye Mtandao wa Jamii
Forum huku akisema suala hilo halihitaji vikao vya chama kulijadili
isipokuwa vyombo vya habari na hususan, mitandao ya kijamii kwani hata
Zitto hutumia mitandao hiyo.
Akijibu hoja hizo, Zitto alisema tangu siku nyingi
alikwisha piga marufuku kwenye Kamati ya Bunge ya Hesabu za Serikali
(PAC) kupokea posho kutoka taasisi au mashirika yanayosimamiwa na kamati
hiyo.
Alisema tangu alipokuwa Mwenyekiti wa Kamati ya
Bunge ya Hesabu za Mashirika ya Umma(POAC), alipiga marufuku posho na
pia aliwahi kuwashtaki Taasisi ya Kupambana na Kuzuia Rushwa (Takukuru)
wabunge wanaochukua posho kutoka taasisi za Serikali.
Ripoti kuhusu Zitto mtandaoni
Zitto pia alipata msukosuko mwingine baada ya
kusambazwa ripoti inayoitwa ‘Taarifa ya Siri ya Chadema’ iliyomtuhumu
kuwa alikuwa anashirikiana na CCM na viongozi wa Idara ya Usalama wa
Taifa kuhujumu chama hicho.
Ripoti hiyo inayodaiwa kuwa iliandaliwa na Idara
ya Upelelezi ya Chadema, ilieleza kuwa Zitto alikuwa akipokea fedha
kutoka kwa maofisa wa usalama na kuzisambaza kwa makada wengine wa chama
hicho ili wafanye kazi ya kukihujumu.
Hata hivyo, Chadema kupitia kwa Mnyika ilitoa taarifa kupinga vikali suala hilo.
CAG kukagua ruzuku
Pia, Zitto aliingia katika malumbano na chama chake baada ya kutuhumu vyama vya siasa kuwa hesabu zake hazikaguliwi na CAG.
Chadema ilipinga vikali madai hayo na kueleza kuwa imekuwa inatumia taasisi binafsi kufanya kazi hiyo.
Mwigamba, Shibuda na uongozi Mara
Suala jingine linalotazamiwa kujadiliwa katika
kikao hicho ni kusimamishwa kwa Mwigamba na Baraza la Uongozi Kanda ya
Kaskazini ambako kulizuka vurugu kiasi cha kunyang’anywa kompyuta
mpakato (laptop) baada ya kudaiwa alikuwa anasambaza taarifa za kuhujumu
chama hicho.
Suala lake linasubiri uamuzi wa kikao cha Kamati Kuu kama lile la kuvunjwa kwa uongozi wa Chadema wa Mara.
Pia kitendo cha Baraza la Kanda ya Ziwa Mashariki
kumtimua Shibuda kwa madai kwamba halina imani naye nacho kina uwezekano
mkubwa wa kujadiliwa. Chanzo: MWANANCHI
0 Responses so far.
Post a Comment