Katibu Mkuu Kiongozi, Balozi Ombeni Sefue
RAIS Jakaya Kikwete amefanya mabadiliko katika Baraza la Mawaziri kujaza nafasi za mawaziri watano walioacha nafasi zao wazi, kutokana na sababu mbalimbali. Katika uteuzi huo, Rais Kikwete ameteua mawaziri wapya wawili na Naibu mawaziri wapya wanane, huku akiwapandisha vyeo naibu mawaziri wanne kuwa mawaziri kamili.
Aidha katika mabadiliko hayo yaliyotangazwa jana na Katibu Mkuu Kiongozi, Balozi Ombeni Sefue, Rais Kikwete amempumzisha kazi waziri mmoja na naibu mawaziri wanne, huku akihamisha mawaziri wawili na naibu mawaziri sita kutoka katika wizara walizokuwa wakitumikia kabla ya mabadiliko. 
Kwa mujibu mabadiliko hayo, waziri pekee aliyepumzishwa kazi ni Dk Terezya Huvisa, ambaye alikuwa Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais (Mazingira). Naibu mawaziri waliopumzishwa kazi ni Gregory Teu, aliyekuwa Naibu Waziri wa Viwanda na Biashara na Philipo Mulugo, aliyekuwa Naibu Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Ufundi.
Wengine ni Benedict Ole-Nangoro aliyekuwa Naibu Waziri wa Maendeleo ya Mifugo na Uvuvi na Goodluck Ole-Medeye, aliyekuwa Naibu Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi.
Kabla ya kupumzishwa kazi kwa mawaziri hao, nafasi zilizokuwa wazi ziliachwa na Balozi Khamis Kagasheki, aliyejiuzulu katika nafasi ya Waziri wa Maliasili na Utalii, kutokana na ripoti ya Operesheni Tokomeza Ujangili, iliyomhusisha na ukiukwaji wa sheria, uliofanywa na watendaji wa chini yake.
Wengine ambao uteuzi wao ulitenguliwa na Rais Kikwete kutokana na ripoti hiyo ni Dk Emmanuel Nchimbi (Mambo ya Ndani ya Nchi), Shamsi Vuai Nahodha (Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa) na Dk David Mathayo (Maendeleo ya Mifugo). Nafasi nyingine iliachwa wazi na aliyekuwa Waziri wa Fedha, Dk William Mgimwa, aliyefariki dunia Afrika Kusini kutokana na maradhi.
Mawaziri wapya ni Dk Asha-Rose Migiro, ambaye alikuwa Naibu Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa na kabla ya hapo Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa. Kwa sasa ameteuliwa kuwa Waziri wa Katiba na Sheria. Katika mabadiliko hayo, Dk Titus Kamani, Mbunge wa Busega ndiye mteule pekee aliyetoka kuwa Mbunge na kuwa Waziri kamili katika Wizara ya Maendeleo ya Mifugo na Uvuvi.
Wengine wapya ambao wameteuliwa kuwa naibu mawaziri ni Mwigulu Nchemba, Naibu Waziri wa Fedha (Sera), Dk Kebwe Stephen, Naibu Waziri, Afya na Ustawi wa Jamii na Jenista Mhagama, Naibu Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Ufundi.
Dk Pindi Chana ameteuliwa kuwa Naibu Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia na Watoto na Kaika Telele, Naibu Waziri wa Maendeleo ya Mifugo na Uvuvi. Wengine ni Godfrey Zambi, kuwa Naibu Waziri Kilimo, Chakula na Ushirika, Juma Nkamia, Naibu Waziri Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo na Mahmoud Mgimwa, Naibu Waziri, Maliasili na Utalii.
Mbali na wateule wapya, Rais Kikwete amewapandisha vyeo naibu mawaziri wanne, akiwemo Saada Mkuya Salum kutoka Naibu Waziri wa Fedha, kuwa Waziri wa Fedha. Mwingine ni Lazaro Nyalandu kutoka Naibu Waziri Maliasili na Utalii kuwa waziri kamili katika wizara hiyo na Dk Seif Seleman Rashidi kutoka Naibu Waziri, Afya na Ustawi wa Jamii mpaka Waziri kamili wizara hiyo hiyo.
Dk Binilith Mahenge yeye amepandishwa cheo na kuhamishwa, kutoka Naibu Waziri wa Maji na kuwa Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais (Mazingira).
Rais Kikwete pia amewahamisha mawaziri wawili, akiwemo Dk Hussein Ali Mwinyi kutoka Waziri wa Afya na Ustawi wa Jamii, kuwa Waziri wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa.
Kwa uhamisho huo, Dk Mwinyi anakuwa na historia ya kuwa Wizara ya Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa mara mbili, kama ilivyo katika Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii, ambako amewahi kuiongoza mara mbili.
Mathias Chikawe aliyekuwa Waziri wa Katiba na Sheria, amehamishwa kwenda kuwa Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi. Naibu mawaziri waliohamishwa ni pamoja na George Simbachawene, kutona Wizara ya Nishati na Madini, kwenda Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi na Amos Makalla kutoka Wazara ya Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo kwenda Wizara ya Maji.
Wengine ni Charles Kitwanga kutoka Ofisi ya Makamu wa Rais, kwenda Wizara ya Nishati na Madini; Adam Malima kutoka Wazara ya Kilimo, Chakula na Ushirika mpaka Wizara ya Fedha.
Pia, Janet Mbene aliyekuwa Naibu Waziri wa Fedha, amehamishiwa Wizara ya Viwanda na Biashara na Ummy Mwalimu, kutoka Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia na Watoto, kwenda Ofisi ya Makamu wa Rais, Mazingira.

photo ,

0 Responses so far.