Na Athumani Issa Hanang'

MWANARIADHA mkongwe nchini, Wilhelm Gidabuday, ametangaza rasmi nia ya kugombea Ubunge katika Jimbo la Hanang’ kwa tiketi ya Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), kwenye uchaguzi mkuu ujao.

Gidabuday ambaye katika siku za hivi karibuni, amejozelea umaarufu kutokana na misimamo yake ya kutetea masilahi ya wanariadha nchini, aliyabainisha hayo juzi katika mazungumzo maalum na Wazalendo 25 Blog.

Alisema baada ya kufikiria kwa makini huku akifuata ushauri wenye busara kutoka kwa wenyeji wa wilaya ya Hanang’, ameamua kuitikia maombi ya wana Hanang.

Baada ya kufikiri na kushauriwa vizuri na watanzania wenye busara wenyeji wa Hanang’ hatimaye nimeamua kutangaza nia yangu ya kuwania nafasi ya Ubunge katika uchaguzi mkuu wa 2015 kupitia Chadema”, alisema Gidabuday.

Gidabuday alisisitiza kwamba uamuzi wake kugombea nafasi ya Ubunge wa Jimbo hilo, ambalo kwa sasa linashikiliwa na Dkt. Mary Nagu (CCM), umetokana na imani kwamba kugombea nafasi yoyote ni haki ya msingi ya kila Mtanzania kikatiba.

“Kabla ya kujitathmini mwenyewe nilifanyiwa tathmini na rika tofauti ndani ya jamii, makundi hayo yakiwakilisha watu wenye busara katika jamii. mimi nilikumbushwa nijitathmini baada ya wao kuniweka katika orodha ya watu wenye sifa stahiki”, alisema.


Alipoulizwa kuhusu uwezo wake katika kutumikia nafasi hiyo, Gidabuday alisema uzoefu wake katika kupigania maendeleo ya michezo nchini kunampa kiburi kuwa akipewa fursa hiyo atawatumikia wananchi wa jimbo lake.


“Wanaonifahamu watanijibia hili, mwaka 2010, niliongoza harakati za kuwaondoa wavamizi wa vyanzo vya maji pembezoni mwa mlima Hanang, upande wa kijiji cha Nangwa, utakumbuka wavamizi wale walijiamini sana sababu kati yao kulikuwa na wajomba zake Mbunge”, alisema Gidabuday.

Katika siku za hivi karibuni, kutokana na misimamo yake na harakati za kupinga rushwa, Gidabuday alijikutana akiingia kwenye mgogoro na viongozi wa shirikisho la riadha nchini (RT), inayoongozwa na Mbunge wa Mvomero, Anthony Mtaka (CCM).

Mwanaharakati amekuwa akiutuhumu uongozi wa RT, kuhusika na michezo michafu ambayo imepelekea mafanikio kiduchu ya Riadha, alisema kazi yake ya kwanza kama Mbunge itakuwa ni kumaliza migogogro ya ardhi kati ya wakulima na wafugaji Jimboni mwake.

“Nitahakikisha natatua tatizo la migogoro ya ardhi yaliyoanza tangu uvamizi wa mashamba ya Gehandu na Bassotu mwishoni mwa 1960 hadi mwanzoni mwa 1980 kwa kile kilichodaiwa kuwa uwekezaji wa shirika la NAFCO la Canada, kufuatilia kesi iliyopo mahakama ya dunia kuhusu haki ya jamii ya Wadatoga maarufu Wabarbaig”, alisema


Aidha mwanariadha huyo ambaye kwa sasa anaendesha mradi wa Ujenzi wa Kijiji cha michezo cha kitaifa (National Sports Village), alisema akiwa Mbunge atahakikisha ujenzi wa kituo hicho ambacho kimekuwa kikiwekewa pingamizi kutokana na mitizamo mbalimbali na tamaa ya wachache, kinakamilika.

Mwanariadha huyo, alisema msukumo wa kuingia bungeni unatokana na hamu ya kuona rasilimali nyingi za wilaya ya Hanang’ zinatumika kuwakomboa wana Hanang’ kuondokana na lundo la umasikini unaowakabili kwa sasa.

“Wilaya ya Hanang ni tajiri sana, ardhi yenye rutuba, mlima wa tatu kwa urefu Tanzania, msitu wenye wanyama adimu duniani (Extinct & Rare Birds), ziwa la chumvi, mifugo na mazao mengi sana! Iweje wanahanang wanaishi maisha wanayoishi sasa kama si uzembe wa viongozi wasio wazalendo?” alihoji

photo ,

0 Responses so far.