Mwanasheria Mshauri na Mtetezi wa Haki za Binadamu Mkoani Morogoro ambaye pia ni Mwasisi wa Blog hii Amani Mwaipaja anatarajia kuzindua vitabu vyake viwili katikati ya mwezi wa Saba. Vitabu Vitakavyozinduliwa ni pamoja na IJUE SHERIA NA HAKI ZAKO na kitabu cha UKWELI USIOPENDWA.
Kwa mujibu wa Mratibu wa tukio hilo-Felista Lyamba, tarehe rasmi ya Uzinduzi itatajwa hapo baadaye. Ifuatayo ni sehemu fupi ya utangulizi wa kitabu cha Ukweli Usiopendwa
Taifa Linaangamia
Tumo
katika taifa lililogubikwa na maswali. Watu hawaoni tena nuru kwa maisha yao ya baadae. Mazungumzo
ya watu barabarani, kwenye vyombo vya usafiri, vyombo vya habari, maofisini,
sehemu za ibada, vijiweni na kwenye mikusanyiko ya watu hujiuliza tunakwenda
wapi. Ugumu wa maisha umewafanya wengine wazikimbie familia zao huku wengine
kwa kuchanganyikiwa wamejiua na kuua wenzao.
Maisha
ya wengi yamekuwa ya kubahatisha na kukata tamaa. Hali ya kukata tamaa
iliyoenea miongoni mwa wananchi wengi haitokani tu na matatizo peke yake wala
maovu katika jamii. Kinachokatisha tamaa zaidi ni kuona viongozi wao walioapa
kuwalinda dhidi ya uovu wakicheka na uovu wenyewe na wakati mwingine
wanakumbatiana na waovu hadharani. Mpaka sasa hakuna dalili kwa viongozi
kumaliza kucheka
Serikali
sasa inakabiliwa na changamoto nyingi kutoka kila upande. Ni kama mfumo mzima
wa utawala umesimama na Mungu ndiye ajuaye nini kitatokea kesho na keshokutwa
ndani ya taifa letu. Nchi inakabiliwa na
tatizo kubwa la ukosefu wa ajira, umasikini uliokithiri, rushwa hususan kwenye
mikataba ya kinyonyaji inayowanufaisha watu wachache katikati ya mamilioni ya
watanzania. Uporaji wa rasilimali za taifa, mishahara midogo isiyoendana na
hali ya maisha, kuporomoka kwa uchumi na huduma mbovu za kijamii ni baadhi tu
ya dalili za ugonjwa hatari uliolikumba taifa.
Ugonjwa
huo umetengeneza matabaka ndani ya taifa moja ndio maana mara kadhaa wanazuoni,
wanasiasa na wananchi wamekuwa wakilalamika na kutaka mabadiliko ya kulikwamua
taifa kutoka hapa lilipo. Ama kwa hakika taifa linaugua, linaugua ugonjwa wa
ajabu.
Serikali,
licha ya kuwa na nguvu kubwa ikitumia polisi, magereza, jeshi la wananchi,
usalama wa taifa na wataalam waliobobea kwenye kila fani nayo imeshindwa
kuwabana wabadhilifu ambao ndio virusi vya ugonjwa huo. Wanafanya wapendavyo
bila kujali shida za watu wengine wakiwa chini ya mwamvuri wa chama cha
mashetani
Ufisadi
unazungumzwa kila mahali, nani asiyepata kusikia habari zake?, vipofu, ingawa
hawaoni lakini maisha wanayoishi na yale wanayoyasikia yanatosha kuwashuhudia
hali ya taifa letu. Bubu, ingawa hawezi kusema na kusikia lakini anayoyaona ni
sauti za ajabu zinazopenya mpaka katika mawazo yake ya ndani.
Mahakimu
wamepotoka, wanahongwa kwa rushwa na kudanganywa. Ulevi, fujo, kukosa uaminifu
wa kila namna kumeshamiri miongoni mwa wale wanaozisimamia sheria. Hivi sasa,
kwasababu chama cha mashetani hakiwezi kuudhibiti ukweli unaowekwa wazi na
wazalendo kila kukicha, sasa kinaendeleza mbinu ya kuwagawa watanzania kwa
dini, rangi, ukabila na hata jinsia. Watawala wanasukumwa na tamaa ya
kulimbikiza mali
na kupenda anasa. Kutokuwa na kiasi kumewapumbaza kiasi kwamba kila mmoja
anafikiria namna ya kujinufaisha yeye mwenyewe kwanza.
Idadi
ya vijana wanaokichukia Chama cha Mashetani nayo inazidi kuongezeka kila
kukicha. Mawakala wa upandikazaji chuki hii ni umasikini, mfumko wa bei,
ukiukwaji wa haki za binadamu, ubambikaji wa kesi dhidi ya watu unaofanywa na jeshi
la polisi, matokeo mabaya ya mitihani ya taifa, huduma mbovu za kijamii na
ubaguzi wa mikopo katika vyuo, ama kwa hakika, tunaangamia kwa kasi ya ajabu na
matokeo ya siku za usoni yatakuwa mabaya zaidi kama hatutachukua hatua za
haraka kulinusuru taifa kutoka kutoka katika utawala wa mashetani.
Leo
hii ikitokea ajali hata ya baiskeli tu, ndani ya muda mfupi mamia ya vijana
wanakusanyika kushangaa kuanzia asubuhi hadi jioni jua linapotua. Wanashangaa
sio kwasababu wanapenda, la hasha, ni kwasababu hawana cha kufanya, wanaweza
kushangaa hata wiki nzima. Hata wale wenye kujiajiri wanaishi maisha ya
kubahatisha. Vijana wengi wanacheza bahati nasibu wakiwa na imani ya kufanikiwa
siku moja kama wanavyohimizwa kupitia mitandao
ya simu za mkononi, wanasema unalala, Unaamka Milionea. Hapa ndipo tulipofika
baada ya safari ya miaka zaidi ya hamsini.
Taifa
linashuhudia ongezeko la vitendo vya rushwa. Rushwa imekuwa ikidaiwa na
kutolewa wakati wa kuwaandikisha watoto wa wanyonge shule. Walimu nao wamekuwa
wakitoa rushwa ili waweze kupandishwa vyeo. Wagonjwa mahospitalini wanalazimika
kutoa rushwa ili waweze kupatiwa dawa na vitanda ingawa huduma si za
kuridhisha. Maofisa biashara nao wanadai rushwa ili kutoa leseni kwa
mfanyabiashara ambaye hata mtaji wake wa biashara tu ni wa wasiwasi. Wanyonge
hawana pa kukimbilia zaidi ya kulalamika kimoyomoyo. Pamoja na hayo yote,
lakini ule mwisho umekaribia, mwisho wa kuangamizwa kwa chama cha mashetani.
0 Responses so far.
Post a Comment