Na Lydia Churi- MAELEZO
Serikali imewasimamisha kazi na itawafungulia mashtaka ya kijeshi Maafisa watano wa Jeshi la Polisi nchini kutokana na tuhuma mbalimbali za ukiukaji wa maadili na taratibu za jeshi hilo.

Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi Dkt. Emmanuel Nchimbi (pichani kulia) amewataja waliosimamishwa kazi kuwa ni  Elias Mwita aliyekuwa Mkuu wa Upelelezi Mkoa wa Mbeya, Jacob Kiango aliyekuwa Msaidizi wa Mkuu wa Upelelezi Mkoa wa Mbeya na Charles Kinyongo aliyekuwa Mkuu wa kikosi cha kutuliza Ghasia Mkoa wa Mbeya.
Dkt. Nchimbi amesema leo jijini Dar es salaam kuwa  viongozi hao wamesimamishwa kazi tangu jana kutokana na kukiuka maadili ya jeshi la Polisi nchini ambapo wanatuhumiwa kwa madai kuwa walipeleka chumvi na sukari kwenye Ofisi ya Mkemia Mkuu badala ya kilo 1.9 ya madawa ya kulevya aina ya Cocaine yaliyokamatwa na askari mkoani Mbeya mwezi Machi mwaka jana.
Waziri Nchimbi alisema vitendo hivyo vinavyofanywa na viongozi wa jeshi la Polisi vinawavunja moyo na kuwapa hofu askari wa ngazi ya chini ambao hushindwa kufanya kazi zao kwa uadilifu unaotakiwa.  
Katika hatua nyingine, aliyekuwa mkuu wa Upelelezi mkoani Kagera Peter Matagi amesimamishwa kazi na atafunguliwa mashtaka ya kijeshi kutokana na kukiuka taratibu za kazi kwa kuwabambikiza kesi zisizo na dhamana wananchi 13 wa kata ya Nyakasimbi wilaya ya Karagwe mkoa wa Kagera Kutokana na vurugu za kugombea ardhi ambazo hazikuwiana na aina ya mashtaka walioshtakiwa hali inayoonesha dalili ya uwepo wa rushwa
Waziri Nchimbi alisema wananchi hao walibambikizwa kesi ya ujambazi wa kutumia silaha ambapo walikaa mahabusu kwa muda wa miezi miwili na baadaye timu ya uchunguzi iliyoongozwa na waziri mwenyewe kugundua kuwa mashtaka waliyoshtakiwa hayakuwa sahihi hali ambayo ilisababisha Mwendesha Mashtaka Mkuu wa Serikali (DPP) aliifuta kesi.
Aidha, Serikali pia imemsimamisha kazi aliyekuwa Mkuu wa Polisi wilaya ya Serengeti Paul Mng’ong’o kwa kosa la kuingia katika Hifadhi ya Mbuga za wanyama ya Serengeti na kupanga njama ya kuchimba madini aina ya dhahabu ndani ya hifadhi hiyo hali iliyosababisha kiongozi huyo kushtakiwa  kwenye mahakama ya kiraia huko Serengeti.
Wakati huo huo Kamishna Msaidizi Mwandamizi wa Polisi aliyekuwa anasimamia ajira katika jeshi hilo nchini Renatus Chalamila amepewa likizo ya mwezi mmoja baada ya kutajwa mara nyingi kuhusika na kuwatoza fedha vijana walioomba ajira ya jeshi la polisi ili awapatie kazi hiyo.
Alisema Chalamila amepewa likizo hiyo na mapendekezo kupelekwa kwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kama mamlaka ya nidhamu  ili Rais afanye maamuzi juu ya tuhuma zinazomkabili askari huyo. 
Kufuatia hali hiyo jeshi la polisi limelazimika kuwaondoa katika mafunzo askari wanafunzi 95 waliokuwa wamejiunga na chuo cha polisi baada ya kubainika kuwa walipata fursa hiyo kwa kutoa fedha.
Waziri Nchimbi alitoa wito kuwa Serikali itawaunga mkono askari wanaofanya kazi kwa uadilifu ila watakaoenda kinyume na maadili na taratibu za jeshi la polisi serikali haitasita kuwachukulia hatua za kisheria ikiwemo kuwafukuza kazi.
Hatua zilizochukuliwa na Serikali kwa viongozi wa jeshi la polisi ni sehemu ya makubaliano ya Maafisa waandamizi wa jeshi la Polisi nchini waliokutana hivi karibuni mjini Dodoma kulinda maadili ya jeshi hilo na kukabiliana na vitendo vyote vinavyolichafua jeshi hilo kwa jamii ili  kutatua kero za wananchi na kuzingatia utawala bora. 
SOURCE: MICHUZI JR

photo

0 Responses so far.