Mkurugenzi Msaidizi wa Habari, Elimu na Mawasiliano wa Bodi ya Mikopo ya Wanafunzi
wa Elimu ya Juu (HESLB) Bw. Cosmas Mwaisobwa (kulia) akiwasilisha
taarifa ya utekelezaji wa majuku ya Bodi kwa Naibu Waziri wa Elimu na
Mafunzo ya Ufundi Mhe. Anne Kilango Malecela leo (Jumatano, Aprili 22,
2015) jijini Dar es Salaam. Naibu Waziri alifanya ziara ya kikazi katika
Bodi hiyo na kukutana na uongozi wa Bodi.
Naibu Waziri wa
Elimu na Mafunzo ya Ufundi Mhe. Anne Kilango Malecela ameilekeza Bodi ya Mikopo
kwa Wanafunzi wa Elimu ya Juu (HESLB) kuongeza kasi ya utoaji elimu kwa wadaiwa
wake na umma kwa ujumla ili kuongeza makusanyo ya marejesho na hatimaye kuwa na
mfuko endelevu wa mikopo ya wanafunzi.
Akizungumza na
uongozi wa Bodi hiyo jijini Dar es Salaam leo (Jumatano, Aprili 22, 2015),
Naibu Waziri Malecela amesema wadaiwa wa Bodi hiyo wakielewa umuhimu wa kulipa
mikopo yao, kasi ya ulipaji itaongezeka.
“Ongezeni juhudi
zaidi na hasa tengenezeni matangazo ya televisheni yanayotoa elimu ili
kuwakumbusha wadaiwa na wananchi kwa ujumla juu umuhimu wa kulipa,” amesema
Naibu Waziri wakati wa ziara yake ya kikazi katika ofisi za Bodi hiyo jijini
Dar es Salaam.
Maelekezo ya Naibu
Waziri yalifuatia taarifa ya utekelezaji wa majukumu ya Bodi iliyowasilishwa na
Naibu Mkurugenzi wa Habari, Elimu na Mawasiliano wa HESLB Bw. Cosmas Mwaisobwa
ambaye alitaja changamoto mbalimbali zinazoikabli HESLB ikiwemo wakopaji wengi na waajiri kutokutoa ushirikiano
kwa Bodi katika urejeshwaji mikopo.
“Wakopaji wengi ambao mikopo yao inapaswa kuanza
kurejeshwa hawatoi ushirikiano wa kutosha kwa Bodi katika kurejesha mikopo yao,
na hili linachangiwa pia na kutokuwepo kwa Vitambulisho vya Kitaifa ambavyo
vingerahisisha ugunduzi wa wapi walipo wadaiwa hao,” amesema Mwaisobwa katika
kikao na Naibu Waziri.
Mwaisobwa alitaja changamoto nyingine kuwa ni pamoja
na mtazamo potofu kuwa fedha zinazotolewa na Bodi hiyo ni ruzuku badala ya
mikopo na kuongezeka kwa idadi ya waombaji mikopo wakiwemo hata wale ambao
wazazi wao wana uwezo wa kuwagharamia.
Kwa mujibu wa Mwaisobwa, changamoto nyingine ni
pamoja na baadhi ya wazazi, walezi na waajiri na wafadhili wenye uwezo kujitoa
katika kugharamia wanafunzi wanaosoma katika taasisi za elimu ya juu kwa
kutegemea mikopo inayotolewa na Bodi.
Pamoja na changamoto hizo, Mwaisobwa, kwa Niaba
ya Mkurugenzi Mtendaji wa Bodi alimweleza Naibu Waziri Malecela kuwa katika
mwaka wa masomo 2014/2015, kati ya
waombaji wa mikopo 39,411 wa mwaka wa kwanza waliofanyiwa tathmini ya
uwezo wa kiuchumi, wanafunzi 33,595 walipangiwa mikopo.
Kati ya hao, amesema Mwaisobwa, wanafunzi 31,238
ni wa shahada ya kwanza katika vyuo vya ndani, 2,117 ni wa wanafunzi wa
Diploma ya Ualimu katika fani ya sayansi na hisabati na wengine 160 ni
wa mwaka wa kwanza wanaosoma nje ya nchi. Wanafunzi 80 ni wa shahada ya
Umahiri na Uzamivu katika vyuo vya ndani ya nchi.
Mikopo hiyo hutolewa ili kugharamia maeneo sita
ambayo ni chakula na malazi; mafunzo kwa vitendo; vitabu na viandikwa; fedha za
utafiti; ada ya mafunzo; na mahitaji maalumu ya kitivo
HESLB ilianzishwa kwa sheria ya Bunge na 9 ya
mwaka 2004 na kuanza kazi rasmi mwezi Julai, 2005 ili, pamoja na majukumu
mengine kutoa mikopo kwa wanafunzi wahitaji waliodahiliwa katika taasisi za
elimu ya juu. Aidha, jukumu jingine la Bodi ni kudai na kukusanya mikopo yote
iliyotolewa kwa wahitimu wa taasisi za elimu ya juu kuanzia mwaka 1994 wakati
Serikali ilipoanza kukopesha wanafunzi.
Kwa mujibu wa Mwaisobwa, jumla ya wanafunzi
291,582 wamenufaika na mikopo ya elimu ya juu inayotolewa na Serikali kati ya
mwaka 1994 na Juni mwaka jana (2014). Jumla ya kiasi cha fedha kilichokopeshwa
hadi kufikia mwaka jana (Juni, 2014) ni Tshs 1.8 trilioni ambapo Tshs 51.1
bilioni zilitolewa na iliyokuwa Wizara ya Elimu Juu, Sayansi na Teknolojia na Tshs
1.75 trilioni zimetolewa na HESLB tangu ilipoanza kazi rasmi Julai 2005
0 Responses so far.
Post a Comment