Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania,
Mheshimiwa Jayaka Mrisho Kikwete amemtumia salamu za pongezi nyingi Rais Mteule
wa Jamhuri ya Kenya, Mheshimiwa Uhuru Kenyatta.
Katika salamu hizo zilizotumwa leo,
Jumamosi, Machi 9, 2013, saa chache baada ya kuthibitishwa rasmi kuwa Mheshimiwa
Kenyatta ameshinda Uchaguzi Mkuu wa Kenya uliofanyika mwanzoni mwa wiki hii
Jumatatu, Machi 4, 2013, Rais Kikwete amemwambia Mheshimiwa Uhuru
Kenyatta:
“Mpendwa Rais Mteule na Kaka, ilikuwa
ni furaha kubwa kwangu kupokea taarifa ya ushindi wako wa kuchaguliwa kuwa Rais
wa Jamhuri ya Kenya. Niruhusu, kwa niaba ya Serikali na Wananchi wa Tanzania, na
kwa hakika, kwa niaba yangu binafsi kukupogenza kwa dhati ya moyo wangu kwa
mafanikio haya makubwa ya kuchaguliwa kwako.”
Ameongeza Rais Kikwete: “ Ushindi huu
ni ushahidi na ishara ya wazi kabisa ya imani na matumaini ambayo wananchi wa
Kenya waliyonayo katika uongozi wako. Huu ni utambuzi wa kazi yako maridadi na
mchango wako mkubwa ambao umeutoa katika nafasi mbali mbali za uongozi katika
siku za nyuma katika jitihada zako za kuleta maendeleo ya kiuchumi na kijamii na
ustawi wa nchi yako na wananchi wake.”
Amesisitiza Rais Kikwete: “Wakati
unajiandaa kuchukua madaraka ya juu zaidi katika nchi yako, napenda
kukuhakikishia msimamo wake binafsi pamoja na ule wa Serikali yangu wa
kuunga mkono Serikali yako. Ni imani yangu kubwa kwamba pamoja tutaweza
kuendelea kusukuma mbele zaidi maendeleo ya nchi zetu – Kenya na Tanzania na pia
utengamano wa Afrika Mashariki kwa manufaa ya nchi zetu na wananchi
wake.”
0 Responses so far.
Post a Comment