Ilikuwa siku mbaya kwa Mfanyabiashara Ahmed Amran raia wa pakistan na wenzake watano walipofikishwa mbele ya mahakama ya hakimu Mkazi jjijini arusha kwa tuhuma za kutrosha nje ya nchi wanyamapori hai 136 wa aina 14 tofauti wenye thamani ya shilingi za kitanzania milioni 170. Kati ya watuhumiwa hao wawili kati yake walikuwa ni maafisa usalama wa uwanja wa ndege wa kimataifa wa Kilimanjaro. Miongoni mwa wanyama wanaotuhumiwa kuwasafirisha ni pamoja na twiga, mnyama ambaye ni moja ya kielelezo cha nembo ya taifa
Maswali mengi yalioulizwa miongoni mwa wananchi ni kwa namna gani watuhumiwa hao waliweza kumsafirisha myama mrefu kama twiga ndani ya ndege mpaka Pakistan pasipo wana usalama lukuki waliopo uwanjani hapo kujua. Kitendo hicho ni ushahidi mzuri tu kuwa taifa letu sasa limegubikwa na ugonjwa hatari wa upungufu wa kinga za uchumi. Maliasili zinaibiwa na hakuna mtu anayejali zaidi ya viongozi kuendelea kuimba wimbo wa nchi yetu masikini. Mabilioni ya fedha yanakombwa pale benki kuu ya taifa lakini pasipo aibu bado viongozi wanaendelea kuimba wimbo wa Nchi yetu ni masikini.
Kwenye madini nako wanakomba madini na kama hiyo haitoshi wanabeba mpaka mchanga na kuusafirisha nje ya nchi kwa ndege kupeleka kwao na bado viongozi wanaendelea na wimbo ule ule wa nchi yetu bado ni masikini. Ama kwa hakika taifa linaangamia, linaangamia kwa upungufu wa kinga za kiuchumi na ndio maana viongozi wanapata jeuri ya kuuza mpaka mbuga zetu za wanyama, fukwe za bahari, wamebakiza kuuza mito, maziwa na milima, tusipochukua hatua za kuwakemea hadharani watauza nchi nzima
Nchi yetu ina utajiri wa kutisha mfano wake hakuna duniani. Mungu aliijaza nchi yetu kwa madini ya thamani kubwa katika ardhi yake na juu yake akajaza milima ya kuvutia, mito itiririshayo maji, viumbe wa kila aina waishio majini na nchi kavu, mbuga za kuvutia zenye wanyama wa kila aina ambao wengine duniani hakuna, misitu ya kijani na mabonde ya kuvutia lakini bado wananchi wake wanaishi katika wimbi kubwa la umasikini.
Nchi yenye misitu na miti ya kila aina lakini watoto wake bado wanakaa chini kwa ukosefu wa madawati. Nchi yenye vyanzo vya maji kila mahali lakini wananchi wake hawana maji safi na salama ya kunywa.
Wakati nchi ikielekea kusimama huku bei za bidhaa zikipaa na kufanya hali ya maisha kuwa ngumu, viongozi wa nchi wanafanya sherehe na familia zao na kufuja mabilioni ya fedha za wananchi bila woga. Wenye akili timamu hawawezi kusherehekea miaka hamsini ya ndoa yao yenye matatizo lukuki huku watoto wao wakiwa katika hali ya mnuno mkali. Huu si wakati tena wa kusherehekea, ni wakati wa kuomboleza, ni wakati wa kufunga na kuliombea taifa litoke katika ugonjwa huu hatari. Ni wakati wa waumini wa dini zote bila kujali tofauti zao za kiimani kuyakemea mashetani yanayorudisha nyuma maendeleo ya wananchi
(Maelezo zaidi yanapatikana ndani ya kitabu changu cha Shukrani kitakachozinduliwa mwishoni wa mwezi wa tatu wamaka 2013)
0 Responses so far.
Post a Comment