Mkurugenzi Msaidizi wa Habari, Elimu na Mawasiliano wa Bodi ya Mikopo ya  Wanafunzi wa Elimu ya Juu (HESLB) Bw. Cosmas Mwaisobwa (kulia) akiwasilisha taarifa ya utekelezaji wa majuku ya Bodi kwa Naibu Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Ufundi Mhe. Anne Kilango Malecela leo (Jumatano, Aprili 22, 2015) jijini Dar es Salaam. Naibu Waziri alifanya ziara ya kikazi katika Bodi hiyo na kukutana na uongozi wa Bodi.

Naibu Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Ufundi Mhe. Anne Kilango Malecela ameilekeza Bodi ya Mikopo kwa Wanafunzi wa Elimu ya Juu (HESLB) kuongeza kasi ya utoaji elimu kwa wadaiwa wake na umma kwa ujumla ili kuongeza makusanyo ya marejesho na hatimaye kuwa na mfuko endelevu wa mikopo ya wanafunzi.
Akizungumza na uongozi wa Bodi hiyo jijini Dar es Salaam leo (Jumatano, Aprili 22, 2015), Naibu Waziri Malecela amesema wadaiwa wa Bodi hiyo wakielewa umuhimu wa kulipa mikopo yao, kasi ya ulipaji itaongezeka.
“Ongezeni juhudi zaidi na hasa tengenezeni matangazo ya televisheni yanayotoa elimu ili kuwakumbusha wadaiwa na wananchi kwa ujumla juu umuhimu wa kulipa,” amesema Naibu Waziri wakati wa ziara yake ya kikazi katika ofisi za Bodi hiyo jijini Dar es Salaam.
Maelekezo ya Naibu Waziri yalifuatia taarifa ya utekelezaji wa majukumu ya Bodi iliyowasilishwa na Naibu Mkurugenzi wa Habari, Elimu na Mawasiliano wa HESLB Bw. Cosmas Mwaisobwa ambaye alitaja changamoto mbalimbali zinazoikabli HESLB ikiwemo wakopaji wengi na waajiri kutokutoa ushirikiano kwa Bodi katika urejeshwaji mikopo.
“Wakopaji wengi ambao mikopo yao inapaswa kuanza kurejeshwa hawatoi ushirikiano wa kutosha kwa Bodi katika kurejesha mikopo yao, na hili linachangiwa pia na kutokuwepo kwa Vitambulisho vya Kitaifa ambavyo vingerahisisha ugunduzi wa wapi walipo wadaiwa hao,” amesema Mwaisobwa katika kikao na Naibu Waziri.
Mwaisobwa alitaja changamoto nyingine kuwa ni pamoja na mtazamo potofu kuwa fedha zinazotolewa na Bodi hiyo ni ruzuku badala ya mikopo na kuongezeka kwa idadi ya waombaji mikopo wakiwemo hata wale ambao wazazi wao wana uwezo wa kuwagharamia.
Kwa mujibu wa Mwaisobwa, changamoto nyingine ni pamoja na baadhi ya wazazi, walezi na waajiri na wafadhili wenye uwezo kujitoa katika kugharamia wanafunzi wanaosoma katika taasisi za elimu ya juu kwa kutegemea mikopo inayotolewa na Bodi.
Pamoja na changamoto hizo, Mwaisobwa, kwa Niaba ya Mkurugenzi Mtendaji wa Bodi alimweleza Naibu Waziri Malecela kuwa katika mwaka wa masomo 2014/2015, kati ya waombaji wa mikopo 39,411 wa mwaka wa kwanza waliofanyiwa tathmini ya uwezo wa kiuchumi, wanafunzi 33,595 walipangiwa mikopo.
Kati ya hao, amesema Mwaisobwa, wanafunzi 31,238 ni wa shahada ya kwanza katika vyuo vya ndani, 2,117 ni wa wanafunzi wa Diploma ya Ualimu katika fani ya sayansi na hisabati na wengine 160 ni wa mwaka wa kwanza wanaosoma nje ya nchi. Wanafunzi 80 ni wa shahada ya Umahiri na Uzamivu katika vyuo vya ndani ya nchi.
Mikopo hiyo hutolewa ili kugharamia maeneo sita ambayo ni chakula na malazi; mafunzo kwa vitendo; vitabu na viandikwa; fedha za utafiti; ada ya mafunzo; na mahitaji maalumu ya kitivo
HESLB ilianzishwa kwa sheria ya Bunge na 9 ya mwaka 2004 na kuanza kazi rasmi mwezi Julai, 2005 ili, pamoja na majukumu mengine kutoa mikopo kwa wanafunzi wahitaji waliodahiliwa katika taasisi za elimu ya juu. Aidha, jukumu jingine la Bodi ni kudai na kukusanya mikopo yote iliyotolewa kwa wahitimu wa taasisi za elimu ya juu kuanzia mwaka 1994 wakati Serikali ilipoanza kukopesha wanafunzi.

Kwa mujibu wa Mwaisobwa, jumla ya wanafunzi 291,582 wamenufaika na mikopo ya elimu ya juu inayotolewa na Serikali kati ya mwaka 1994 na Juni mwaka jana (2014). Jumla ya kiasi cha fedha kilichokopeshwa hadi kufikia mwaka jana (Juni, 2014) ni Tshs 1.8 trilioni ambapo Tshs 51.1 bilioni zilitolewa na iliyokuwa Wizara ya Elimu Juu, Sayansi na Teknolojia na Tshs 1.75 trilioni zimetolewa na HESLB tangu ilipoanza kazi rasmi Julai 2005

photo ,

0 Responses so far.