Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Mohammed Gharib Bilal, akizungumza na Waziri wa Katiba na Sheria, Dkt. Asha-Rose Migiro, wakati alipofika Ofisini kwake kwa Makamu Ikulu Dar es Salaam, leo kwa mazungumzo. 
Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Mohammed Gharib Bilal, akizungumza na Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Ufundi, Dkt. Shukuru Kawambwa na Waziri wa Mawasiliano, Sayansi na Teknolojia, Prof Makame Mbarawa (katikati) wakati walipofika Ofisini kwake kwa Makamu Ikulu Dar es Salaam. Picha na OMR

photo ,


Jakaya Mrisho Kikwete akipokea kitabu cha Mandela toka kwa Mkurugenzi wa Programu wa Spintelligent ya Afrika Kusini Bi. Amore Swart baada ya kufungua rasmi kongamano la Kilimo Afrika Mashariki katika hoteli ya Serena jijini Dar es salaam Januari 28, 2014.
Rais Jakaya Mrisho Kikwete akipata maelezo toka kwa Bi Meab Mdimi wa Kampuni ya Kilimo ya TECHNOSERVE  baada ya kufungua rasmi kongamano la Kilimo Afrika Mashariki katika hoteli ya Serena jijini Dar es salaam.
Rais Jakaya Mrisho Kikwete akipata maelezo katika banda la Mpango wa Kuendeleza Sekta ya Kilimo Kusini mwa Ukanda wa Afrika (SAGCOT)    baada ya kufungua rasmi kongamano la Kilimo Afrika Mashariki katika hoteli ya Serena jijini Dar es salaam.
Rais Jakaya Mrisho Kikwete akihutubia wakati wa kufungua rasmi kongamano la Kilimo Afrika Mashariki katika hoteli ya Serena jijini Dar es salaam.PICHA NA IKULU

photo ,


Mhe. Tundu Lissu ambae ni kiongozi wa M4C -PAMOJA DAIMA kanda ya Kaskazini akiwa na Kamanda Daniel Urioh (Kulia) ,ambae anatarajia kuchukua Udiwani kata ya Olasiti 2015.
Chopa ikitua katika viwanja vya Sombetini-Jijini Arusha
Mama mzazi wa Diwani mtarajiwa wa CHADEMA Bw. Ally Bananga akiwa katika harakati za kumsapoti mwanae kwenye kampeni.

Mwenyekiti wa BAVICHA Taifa Bw. John Heche akimnadi mgombea wa Udiwani  kata ya Sombetini jijini Arusha
Aliyekuwa diwani wa kata ya Sombetini Bw. Alfonso Mawazo akimweleza Bw. John Heche imani yake kwa Ally Bananga agombee Udiwani  kata ya Sombetini.
Mhe. Tundu Lissu ambae ni kiongozi wa M4C -PAMOJA DAIMA kanda ya Kaskazini akimnadi mgombea wa Udiwani  kata ya Sombetini jijini Arusha.


Mhe. Ephata Nanyaro ambae ni Mwenyekiti wa BAVICHA wilaya ya Arusha Mjini, akimnadi mgombea wa Udiwani  kata ya Sombetini Bw. Ally Bananga.
Bw. Amani Golugwa ambae ni Mratibu wa CHADEMA kanda ya kaskazini, akimnadi mgombea wa Udiwani  kata ya Sombetini Bw. Ally Bananga.
Mhe. Joshua Nassari ambae ni Mbunge wa Arumeru Mashariki akimnadi mgombea wa Udiwani  kata ya Sombetini Bw. Ally Bananga.
Chopa ikiondoka katika viwanja vya sombetini Jijini Arusha.
Wananchi wakiishangilia CHOPA inavyoondoka katika viwanja vya Sombetini Jijini ,Arusha. Picha Zote na Gadiola Emanuel

photo ,


Rais Dkt.Jakaya Mrisho Kikwete akiwa na baadhi ya viongozi wa madhehebu mbalimbali ya Dini waliohudhuria Kongamano la siku mbili linalohusu Rasilimali za Gesi Asilia, Mafuta na Madini kwa Amani na Maendeleo ya Tanzania linalofanyika katika hoteli ya White Sands jijini Dar es Salaam.

HOTUBA YA MHESHIMIWA JAKAYA MRISHO KIKWETE, RAIS WA JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA, WAKATI WA UFUNGUZI WA...

photo

Katibu Mkuu Kiongozi, Balozi Ombeni Sefue
RAIS Jakaya Kikwete amefanya mabadiliko katika Baraza la Mawaziri kujaza nafasi za mawaziri watano walioacha nafasi zao wazi, kutokana na sababu mbalimbali. Katika uteuzi huo, Rais Kikwete ameteua mawaziri wapya wawili na Naibu mawaziri wapya wanane, huku akiwapandisha vyeo naibu mawaziri wanne kuwa mawaziri kamili.
Aidha katika mabadiliko hayo yaliyotangazwa jana na Katibu Mkuu Kiongozi, Balozi Ombeni Sefue, Rais Kikwete amempumzisha kazi waziri mmoja na naibu mawaziri wanne, huku akihamisha mawaziri wawili na naibu mawaziri sita kutoka katika wizara walizokuwa wakitumikia kabla ya mabadiliko. 
Kwa mujibu mabadiliko hayo, waziri pekee aliyepumzishwa kazi ni Dk Terezya Huvisa, ambaye alikuwa Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais (Mazingira). Naibu mawaziri waliopumzishwa kazi ni Gregory Teu, aliyekuwa Naibu Waziri wa Viwanda na Biashara na Philipo Mulugo, aliyekuwa Naibu Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Ufundi.
Wengine ni Benedict Ole-Nangoro aliyekuwa Naibu Waziri wa Maendeleo ya Mifugo na Uvuvi na Goodluck Ole-Medeye, aliyekuwa Naibu Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi.
Kabla ya kupumzishwa kazi kwa mawaziri hao, nafasi zilizokuwa wazi ziliachwa na Balozi Khamis Kagasheki, aliyejiuzulu katika nafasi ya Waziri wa Maliasili na Utalii, kutokana na ripoti ya Operesheni Tokomeza Ujangili, iliyomhusisha na ukiukwaji wa sheria, uliofanywa na watendaji wa chini yake.
Wengine ambao uteuzi wao ulitenguliwa na Rais Kikwete kutokana na ripoti hiyo ni Dk Emmanuel Nchimbi (Mambo ya Ndani ya Nchi), Shamsi Vuai Nahodha (Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa) na Dk David Mathayo (Maendeleo ya Mifugo). Nafasi nyingine iliachwa wazi na aliyekuwa Waziri wa Fedha, Dk William Mgimwa, aliyefariki dunia Afrika Kusini kutokana na maradhi.
Mawaziri wapya ni Dk Asha-Rose Migiro, ambaye alikuwa Naibu Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa na kabla ya hapo Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa. Kwa sasa ameteuliwa kuwa Waziri wa Katiba na Sheria. Katika mabadiliko hayo, Dk Titus Kamani, Mbunge wa Busega ndiye mteule pekee aliyetoka kuwa Mbunge na kuwa Waziri kamili katika Wizara ya Maendeleo ya Mifugo na Uvuvi.
Wengine wapya ambao wameteuliwa kuwa naibu mawaziri ni Mwigulu Nchemba, Naibu Waziri wa Fedha (Sera), Dk Kebwe Stephen, Naibu Waziri, Afya na Ustawi wa Jamii na Jenista Mhagama, Naibu Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Ufundi.
Dk Pindi Chana ameteuliwa kuwa Naibu Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia na Watoto na Kaika Telele, Naibu Waziri wa Maendeleo ya Mifugo na Uvuvi. Wengine ni Godfrey Zambi, kuwa Naibu Waziri Kilimo, Chakula na Ushirika, Juma Nkamia, Naibu Waziri Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo na Mahmoud Mgimwa, Naibu Waziri, Maliasili na Utalii.
Mbali na wateule wapya, Rais Kikwete amewapandisha vyeo naibu mawaziri wanne, akiwemo Saada Mkuya Salum kutoka Naibu Waziri wa Fedha, kuwa Waziri wa Fedha. Mwingine ni Lazaro Nyalandu kutoka Naibu Waziri Maliasili na Utalii kuwa waziri kamili katika wizara hiyo na Dk Seif Seleman Rashidi kutoka Naibu Waziri, Afya na Ustawi wa Jamii mpaka Waziri kamili wizara hiyo hiyo.
Dk Binilith Mahenge yeye amepandishwa cheo na kuhamishwa, kutoka Naibu Waziri wa Maji na kuwa Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais (Mazingira).
Rais Kikwete pia amewahamisha mawaziri wawili, akiwemo Dk Hussein Ali Mwinyi kutoka Waziri wa Afya na Ustawi wa Jamii, kuwa Waziri wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa.
Kwa uhamisho huo, Dk Mwinyi anakuwa na historia ya kuwa Wizara ya Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa mara mbili, kama ilivyo katika Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii, ambako amewahi kuiongoza mara mbili.
Mathias Chikawe aliyekuwa Waziri wa Katiba na Sheria, amehamishwa kwenda kuwa Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi. Naibu mawaziri waliohamishwa ni pamoja na George Simbachawene, kutona Wizara ya Nishati na Madini, kwenda Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi na Amos Makalla kutoka Wazara ya Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo kwenda Wizara ya Maji.
Wengine ni Charles Kitwanga kutoka Ofisi ya Makamu wa Rais, kwenda Wizara ya Nishati na Madini; Adam Malima kutoka Wazara ya Kilimo, Chakula na Ushirika mpaka Wizara ya Fedha.
Pia, Janet Mbene aliyekuwa Naibu Waziri wa Fedha, amehamishiwa Wizara ya Viwanda na Biashara na Ummy Mwalimu, kutoka Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia na Watoto, kwenda Ofisi ya Makamu wa Rais, Mazingira.

photo ,


Rais Dkt.Jakaya Mrisho Kikwete akimjulia hali Waziri Mkuu Msaafu Mzee Cleopa David Msuya aliyelazwa katika hospitali ya Taifa Muhimbili jana jijini Dar es Salaam.
Rais Dkt.Jakaya Mrisho Kikwete na mkewe Mama Salma Kikwete wakimjulia hali Waziri wa nchi Afisi ya Rais Kazi na Utumishi wa Umma wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar(SMZ) Bwana Haroun Ali Suleiman aliyelazwa katika Hospitali ya Taifa Muhimbili jijini Dar es Salaam, Jana (Jumanne)(picha na Freddy Maro).

photo


Mwandishi wa habari na mmiliki wa blog ya Bertha Blog Bi. Bertha Mollel (wa kike mbele) akibeba jeneza lenye mwili wa mwandishi wa habari wa gazeti la Habari Leo Mkoani Manyara, marehemu Fortunatha Ringo aliyefariki dunia Januari 10 mwaka huu jijini Dar es salaam kwa ugonjwa wa kuishiwa damu na kuzikwa Januari 13 kwenye kijiji cha Mdawi Old Moshi.
Jeneza lenye mwili wa mwandishi wa habari wa gazeti la Habari Leo Mkoani Manyara, marehemu Fortunatha Ringo aliyefariki dunia Januari 10 mwaka huu jijini Dar es salaam kwa ugonjwa wa kuishiwa damu, likiingizwa kaburini na kuzikwa Januari 13 kwenye kijiji cha Mdawi Old Moshi.
Mwandishi wa gazeti la Mwananchi mkoa wa Manyara, Joseph Lyimo (kushoto) na Meneja wa Radio Safina ya Arusha, Jovin Msuya wakiweka shada la maua kwenye kaburi la marehemu Fortunatha Ringo, mwandishi wa habari wa gazeti la Habari Leo Mkoani Manyara aliyefariki Januari 10 jijin Dar es salaam na kuzikwa Januari 13 kijijini Mdawi Old Moshi. Na Wazalendo 25 Blog

photo

Hii ni habari mbaya kwa Taifa lenye sifa ya Amani Tanzania watu wake wamegeuka wanyama na kuchukua maamuzi mikononi.Leo asubuhi basi la kampuni ya Mtei toka Arusha limechomwa moto maeneo ya Njia panda mnadani singida baada ya basi hilo kugonga pikipiki yaani bodaboda na kuua watu watatu Hapo hapo.

photo

Aida Nakawala 25 mkazi wa kijiji cha Chiwanda Wilaya ya Momba Mkoa wa Mbeya, hivi karibuni alijifungua watoto wanne  mapacha kwa mkupuo(Quadliplets) katika usiku wa kuamkia Mwaka mpya anaendelea vizuri.
Mwanamke huyo ambaye kwa hivi sasa anaendelea na matibabu katika Hospitali ya Wazazi ya Meta akiwa na watoto wake wote wanne alijifungua majira ya saa 10 alfajiri usiku wa kuamkia Januari Mosi Mwaka huu katika Hospitali ya Wilaya ya Mbozi na watoto wakiwa na uzito wa kawaida tofauti na matarajio ya Wengi. SOMA ZAIDI MBEYA YETU BLOG

photo ,

Picha ya Maktaba ikimwonyesha Waziri wa Fedha, marehemu Dk William Mgimwa akisoma bajeti ya wizara yake bungeni. 

Dar es Salaam na Iringa. Waziri wa Fedha na Mbunge wa Kalenga (CCM), Iringa, William Mgimwa amefariki dunia jana katika Hospitali ya Kloof Medi-Clinic, Pretoria, Afrika Kusini alikokuwa akitibiwa.
Habari zilizopatikana jana kutoka Ubalozi wa Tanzania nchini Afrika Kusini kupitia kwa Msemaji wake, Habib Awesi zilisema Waziri Mgimwa amefariki dunia mchana... “Ni kweli amefariki leo mchana tumepeleka taarifa Ikulu, Dar es Salaam.”
Baadaye jana, Katibu Mkuu Kiongozi, Balozi Ombeni Sefue alithibitisha kupokea taarifa za kifo hicho na kusema Waziri Mgimwa alifariki dunia saa 5:20 kwa saa za Afrika Kusini (saa 6:20).
“Kinachofanyika kwa sasa ni maandalizi ya kuurudisha nyumbani mwili wa marehemu na hilo linafanywa na Serikali kwa kushirikiana na familia yake. Taarifa zaidi zitatolewa baadaye kadiri zitakavyopatikana,” alisema Balozi Sefue.
Akizungumzia msiba huo, Naibu Spika wa Bunge, Job Ndugai alisema: “Bunge limepokea kwa masikitiko taarifa za kifo cha Dk Mgimwa, alikuwa ni mtu mwaminifu katika kazi zake na alishirikiana kikamilifu na wabunge katika kutekeleza kazi za Serikali. Taifa limepoteza mtu makini aliyefanya kazi katika sekta ambayo aliisomea, jambo ambalo lilimfanya awe na ufahamu mzuri wa mambo katika wizara (Fedha),” alisema Ndugai.
Kikwete atuma rambirambi
Jana jioni Rais Jakaya Kikwete alitoa taarifa akielezea kushtushwa na kifo cha Waziri Mgimwa.
“Nimepokea kwa mshtuko na huzuni kubwa taarifa za kifo cha Waziri wa Fedha, Dk William Mgimwa,” ilisema taarifa yake kupitia Kurugenzi ya Mawasiliano, Ikulu.
Alisema taifa limempoteza Waziri Mgimwa katika kipindi lilipokuwa linamhitaji zaidi kutokana na mchango wake mkubwa ambao amekuwa akiutoa kupitia nafasi zake za Waziri wa Serikali na mwakilishi wa wananchi wa Jimbo la Kalenga.
Katika salamu zake kupitia kwa Waziri Mkuu, Mizengo Pinda na kwa familia ya marehemu Mgimwa, Rais Kikwete alisema: “Sina maneno ya kutosha kuelezea mshtuko na huzuni yangu kubwa kufuatia taarifa za kifo cha Mgimwa.
“Binafsi nilimtembelea mara mbili hospitali alikokuwa amelazwa na mara ya mwisho hali yake ilikuwa imeimarika. Tulizungumza kwa kiasi cha dakika 10 hivi akanielezea nia yake na tamaa yake ya kurejea nyumbani kwa sababu hali yake ilikuwa nzuri.
“Sote tunajua mchango wake katika Serikali. Sote tulitamani kuendelea kuwa naye, lakini haya ni mapenzi ya Mungu... Natoa pole nyingi na rambirambi zangu za dhati kwa wana familia wote kwa kuondokewa na mhimili wao. Naungana nanyi katika kuomboleza msiba huo mkubwa. Napenda mjue kuwa msiba huu ni msiba wangu pia. Machungu yenu ni majonzi yangu,” alisema Rais Kikwete.
Jimboni
Mwenyekiti wa Halmashauri ya Iringa Vijijini, Steven Muhapa alisema jana kuwa wamepokea kwa mshituko kifo cha mbunge wao.
Muhapa alisema halmashauri yake imepata pigo la mwaka, kwani walikuwa na mipango mingi ya kutekeleza chini marehemu Mgimwa lakini sasa imeyeyuka... “Alisaidia sana kutuletelea wafadhili kutekeleza ahadi mbalimbali alizoahidi... ni mapenzi ya Mungu.”
Mbunge wa Iringa Mjini (Chadema), Peter Msigwa alisema Mkoa wa Iringa umepoteza mtu muhimu, mahiri na mchapakazi... “Pamoja na kwamba alikuwa CCM, hakubagua mtu. Niliwahi kumpa ushauri mara kadhaa akauchukua ushauri wangu na kuufanyia kazi.”
Mwenyekiti PAC
Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Hesabu za Serikali (PAC), Zitto Kabwe amemwelezea marehemu kwamba alikuwa ni mtu mnyenyekevu na hakuwa na ubaguzi katika kutekeleza wajibu wake akiwa kiongozi wa Serikali.
“Kwa kipindi kifupi nilichofanya naye kazi kwa karibu, kwanza kwenye Kamati ya Fedha, nikiwa mkaribishwa kama Waziri wa Fedha kivuli, kisha kwenye kamati ndogo niliyounda kuhusu miradi ya umeme ya Mchuchuma, Liganga na Ngaka na baadaye akiwa Waziri wa Fedha, jambo la msingi nililoliona kwake ni unyenyekevu na heshima kubwa aliyonayo kwa watu wengine.
“Hakusita kuomba ushauri licha ya kuwa na tofauti za kivyama na kwa kweli ni Waziri wa Fedha niliyeelewana naye zaidi kuliko wengine wote waliopita nikiwa ama Waziri Kivuli au Mwenyekiti wa Kamati za Hesabu.”
Imeandikwa na Raymond Kaminyoge, Florence Majani, Joseph Zablon (Dar) na Geofrey Nyang’oro (Iringa). CHANZO -MWANANCHI

photo , ,