Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Mohammed Gharib Bilal akiwa na Rais mpya wa Malawi Prof. Arthur Peter Mutharika wakiwa katika picha ya pamoja baada ya rais mpya wa Malawi kukabidhiwa madaraka leo jijini Brantyre kwenye hoteli Sunbird. Baada ya kukutana viongozi hao walipata fursa ya kuzungumzia masuala la kidiplomasia baina ya nchi hizi mbili na kukubaliana kuendelea kuwa na mahusiano mema kama nchi zinazoishi ndugu na jirani. Picha kwa Hisani ya Ikulu ya Malawi
***************************************
MAKAMU WA RAIS ASHIRIKI SHEREHE ZA MAKABIDHIANO YA URAIS NCHINI MALAWI
Makamu  wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania DkT. Mohammed Gharib Bilal, Jumatatu Juni 02, 2014 ameshiriki katika sherehe za kukabidhi madaraka kwa Rais mpya wa Malawi Profesa Arthur Peter Mutharika katika sherehe zilizofanyika kwenye uwanja wa Kamuzu Banda jijini Blantyre. Sherehe hizo pia zilihudhuriwa na Rais wa Botswana sambamba na wawakilishi wa nchi za Zimbabwe, Msumbiji, Afrika Kusini na nyinginezo.
Akihutubia baada ya kukabidhiwa sime ambayo ni ishara ya kuwa kiongozi wa watu wa Malawi, Rais Mteule Mutharika alisisitiza kuwa, katika kipindi cha utawala wake atahakikisha kuwa anaifanyia makubwa Malawi sambamba na uhakikisha kuwa anaifanya Malawi itimize majukumu yake ya kimataifa kufuatia kutambua kuwa kujitenga kunaweza kuifanya Malawi kutonufaika na fursa zilizopo duniani.
“Nchi hii ipo katika dunia na siyo rahisi tena kuwa na fikra kwamba Malawi inaweza kubaki peke yake kama kisiwa. Tunahitaji kuwa na wenzetu wa kusaidia maendeleo ya Malawi. Tunawahitaji wahisani toka Kusini ama Mashariki, tunayahitaji mataifa tajiri na mataifa yanayoendelea. Tutafanikiwa sana kama tutaendeleza urafiki kwa wote. Tufanye hivi bila kujali kuwa sisi ni taifa kwani hali ya sasa inahitaji kila mmoja wetu kushirikiana na mwenzake,” alisema.
Katika hotuba hiyo pia amesisitiza kuwa kipindi chake cha utawala atajitahidi kukabiliana na rushwa na kwamba hatakuwa na mchezo kwa wala rushwa katika kipindi akiwa madarakani. Pia alisisitiza kuhusu umuhimu wa kuiunganisha Malawi kwa miundombinu bora ili kuboresha maisha ya wananchi sambamba na kusogeza huduma za wananchi karibu.
Rais Mutharika aliapishwa juzi baada ya kuwashinda washindani wake akiwemo Rais aliyemaliza kipindi chake Joyce Banda ambaye hata hivyo hakuweza kutokea katika sherehe hizi za kukabidhi madaraka. Akizungumzia suala la kutohudhuria kwa Rais Banda, Rais Mteule Mutharika alisema alitegemea Rais Banda kuwepo lakini hakufika nay eye anatambua kuwa wakati wa uchaguzi kulikuwa na tofauti baina yao lakini kwa sasa uchaguzi umeisha na amesahau yaliyopita ili kuanza ukurasa mpya wa kuijenga Malawi. Katika shughuli hiyo pia Rais wa zamani wa Malawi Kamuzu Banda alihudhuria.
Makamu wa Rais Dkt. Bilal na msafara wake walitarajiwa kurejea nyumbani, hii Jumatatu mara tu baada ya kukamilika kwa kazi hii ya makabidhiano.
 Imetolewa na: Ofisi ya Makamu wa Rais
Juni 02, 2014 Blantyre, Malawi

photo ,

0 Responses so far.