Mwanasheria Mshauri na Mtetezi wa Haki za Binadamu Mkoani Morogoro ambaye pia ni Mwasisi wa Blog hii Amani Mwaipaja anatarajia kuzindua vitabu vyake viwili katikati ya mwezi wa Saba. Vitabu Vitakavyozinduliwa ni pamoja na IJUE SHERIA NA HAKI ZAKO na kitabu cha UKWELI USIOPENDWA.

Kwa mujibu wa Mratibu wa tukio hilo-Felista Lyamba, tarehe rasmi ya Uzinduzi itatajwa hapo baadaye. Ifuatayo ni sehemu fupi ya utangulizi wa kitabu cha Ukweli Usiopendwa


Taifa Linaangamia

Tumo katika taifa lililogubikwa na maswali. Watu hawaoni tena nuru kwa maisha yao ya baadae. Mazungumzo ya watu barabarani, kwenye vyombo vya usafiri, vyombo vya habari, maofisini, sehemu za ibada, vijiweni na kwenye mikusanyiko ya watu hujiuliza tunakwenda wapi. Ugumu wa maisha umewafanya wengine wazikimbie familia zao huku wengine kwa kuchanganyikiwa wamejiua na kuua wenzao.

Maisha ya wengi yamekuwa ya kubahatisha na kukata tamaa. Hali ya kukata tamaa iliyoenea miongoni mwa wananchi wengi haitokani tu na matatizo peke yake wala maovu katika jamii. Kinachokatisha tamaa zaidi ni kuona viongozi wao walioapa kuwalinda dhidi ya uovu wakicheka na uovu wenyewe na wakati mwingine wanakumbatiana na waovu hadharani. Mpaka sasa hakuna dalili kwa viongozi kumaliza kucheka

Serikali sasa inakabiliwa na changamoto nyingi kutoka kila upande. Ni kama mfumo mzima wa utawala umesimama na Mungu ndiye ajuaye nini kitatokea kesho na keshokutwa ndani ya taifa letu.  Nchi inakabiliwa na tatizo kubwa la ukosefu wa ajira, umasikini uliokithiri, rushwa hususan kwenye mikataba ya kinyonyaji inayowanufaisha watu wachache katikati ya mamilioni ya watanzania. Uporaji wa rasilimali za taifa, mishahara midogo isiyoendana na hali ya maisha, kuporomoka kwa uchumi na huduma mbovu za kijamii ni baadhi tu ya dalili za ugonjwa hatari uliolikumba taifa.

Ugonjwa huo umetengeneza matabaka ndani ya taifa moja ndio maana mara kadhaa wanazuoni, wanasiasa na wananchi wamekuwa wakilalamika na kutaka mabadiliko ya kulikwamua taifa kutoka hapa lilipo. Ama kwa hakika taifa linaugua, linaugua ugonjwa wa ajabu.

Serikali, licha ya kuwa na nguvu kubwa ikitumia polisi, magereza, jeshi la wananchi, usalama wa taifa na wataalam waliobobea kwenye kila fani nayo imeshindwa kuwabana wabadhilifu ambao ndio virusi vya ugonjwa huo. Wanafanya wapendavyo bila kujali shida za watu wengine wakiwa chini ya mwamvuri wa chama cha mashetani

Ufisadi unazungumzwa kila mahali, nani asiyepata kusikia habari zake?, vipofu, ingawa hawaoni lakini maisha wanayoishi na yale wanayoyasikia yanatosha kuwashuhudia hali ya taifa letu. Bubu, ingawa hawezi kusema na kusikia lakini anayoyaona ni sauti za ajabu zinazopenya mpaka katika mawazo yake ya ndani.

Mahakimu wamepotoka, wanahongwa kwa rushwa na kudanganywa. Ulevi, fujo, kukosa uaminifu wa kila namna kumeshamiri miongoni mwa wale wanaozisimamia sheria. Hivi sasa, kwasababu chama cha mashetani hakiwezi kuudhibiti ukweli unaowekwa wazi na wazalendo kila kukicha, sasa kinaendeleza mbinu ya kuwagawa watanzania kwa dini, rangi, ukabila na hata jinsia. Watawala wanasukumwa na tamaa ya kulimbikiza mali na kupenda anasa. Kutokuwa na kiasi kumewapumbaza kiasi kwamba kila mmoja anafikiria namna ya kujinufaisha yeye mwenyewe kwanza.

Idadi ya vijana wanaokichukia Chama cha Mashetani nayo inazidi kuongezeka kila kukicha. Mawakala wa upandikazaji chuki hii ni umasikini, mfumko wa bei, ukiukwaji wa haki za binadamu, ubambikaji wa kesi dhidi ya watu unaofanywa na jeshi la polisi, matokeo mabaya ya mitihani ya taifa, huduma mbovu za kijamii na ubaguzi wa mikopo katika vyuo, ama kwa hakika, tunaangamia kwa kasi ya ajabu na matokeo ya siku za usoni yatakuwa mabaya zaidi kama hatutachukua hatua za haraka kulinusuru taifa kutoka kutoka katika utawala wa mashetani.

Leo hii ikitokea ajali hata ya baiskeli tu, ndani ya muda mfupi mamia ya vijana wanakusanyika kushangaa kuanzia asubuhi hadi jioni jua linapotua. Wanashangaa sio kwasababu wanapenda, la hasha, ni kwasababu hawana cha kufanya, wanaweza kushangaa hata wiki nzima. Hata wale wenye kujiajiri wanaishi maisha ya kubahatisha. Vijana wengi wanacheza bahati nasibu wakiwa na imani ya kufanikiwa siku moja kama wanavyohimizwa kupitia mitandao ya simu za mkononi, wanasema unalala, Unaamka Milionea. Hapa ndipo tulipofika baada ya safari ya miaka zaidi ya hamsini.

Taifa linashuhudia ongezeko la vitendo vya rushwa. Rushwa imekuwa ikidaiwa na kutolewa wakati wa kuwaandikisha watoto wa wanyonge shule. Walimu nao wamekuwa wakitoa rushwa ili waweze kupandishwa vyeo. Wagonjwa mahospitalini wanalazimika kutoa rushwa ili waweze kupatiwa dawa na vitanda ingawa huduma si za kuridhisha. Maofisa biashara nao wanadai rushwa ili kutoa leseni kwa mfanyabiashara ambaye hata mtaji wake wa biashara tu ni wa wasiwasi. Wanyonge hawana pa kukimbilia zaidi ya kulalamika kimoyomoyo. Pamoja na hayo yote, lakini ule mwisho umekaribia, mwisho wa kuangamizwa kwa chama cha mashetani.

photo

0 Responses so far.