Na Absalom Kibanda

HAKUNA shaka hata kidogo kwamba Chama Cha Mapinduzi (CCM) kinaugua maradhi mabaya kabisa ya uongozi ambayo yamekuwa yakikitafuna chama hicho kwa miaka mingi sasa.

Maradhi haya ya uongozi ambayo CCM inaugua hayakuanza leo na niseme wazi kabisa, hayakuanza wakati huu chama hicho kinapoongozwa na Rais Jakaya Kikwete ambaye ndiye mwenyekiti wake wa taifa.

Ushahidi wa kihistoria unaonyesha kwamba, maradhi hayo ambayo yamepewa majina tofauti na wachambuzi mbalimbali, yalianza kukitafuna chama hicho wakati kikiongozwa na mwenyekiti wake wa kwanza, Baba wa Taifa Mwalimu Julius Nyerere.

Kumbukumbu zinaonyesha kwamba, mara baada ya Nyerere kuamua kustaafu urais mwaka 1985 aliendelea kushikilia madaraka ya mwenyekiti wa CCM kwa takriban miaka mitano zaidi.

Wakati akichukua uamuzi huo, kwa makusudi na kwa kutambua haja ya CCM kujijenga, alifanya ziara nchi nzima akisema anafanya hivyo kwa makusudi mahususi ya kukiimarisha chama.

Ni wazi kwamba hatua ya Mwalimu na viongozi wenzake wa CCM wa wakati huo ilichangiwa kwa kiwango kikubwa na kubaini kwao kuwapo kwa nyufa na udhaifu wa kiuongozi ndani ya chama hicho.

Hata baada ya kufikia hatua ya kuamua kustaafu uenyekiti wa chama hicho na kumwachia aliyekuwa rais wa wakati huo, Ali Hassan Mwinyi, Baba wa Taifa kwa nyakati tofauti alipata kutoa kauli ambazo zilikuwa zikitoa mwelekeo wa wazi uliokuwa ukionyesha kuwapo kwa kasoro kadha wa kadha za kiuongozi ndani ya chama hicho.

Miongoni mwa kauli hizo ni pamoja na zile za kukifananisha chama hicho na kokoro ambalo hutumiwa na wavuvi kuvua samaki kwa namna kukusanya kila takataka na wakati mwingine kusababisha uharibifu mkubwa kwa viumbe vinavyoishi majini.

Si hilo tu, baadhi ya wana CCM wanakumbuka namna Mwalimu alivyofikia hatua ya kusema maneno mazito ambayo yamebandikwa katika kuta za vyumba vya mikutano na ofisi za viongozi wa chama hicho tawala; ‘‘Bila CCM Madhubuti Nchi Itayumba’’.

Kumbukumbu zinaonyesha kwamba, Baba wa Taifa alitamka maneno hayo wakati ule alipokuwa akikinyoshea kidole chama chake hicho hata kufikia hatua ya kukilaani, kukikea na hata kukaribia kabisa kukikana pale aliposema; “CCM si baba yangu wala mama yangu naweza kukihama”.

Ni jambo la bahati mbaya sana kwamba, hofu, wasiwasi na mashaka yaliyopata kuonyeshwa kwa nyakati tofauti na Baba wa Taifa kuhusu CCM, chama alichokiasisi na akakipigania kwa moyo wake wote havijapata kutoweka au kutafutiwa tiba ya kudumu.

Maradhi ambayo Baba wa Taifa alipata kuyasema kuwa yanakitafuna chama hicho yameendelea kubakia kama yalivyo na kwa bahati mbaya zaidi mengi kama si yote yamezidi kuota mizizi na kustawi.

Ni kwa sababu ya maradhi hayo ambayo Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe ameyafananisha na saratani ya damu iliyosambaa katika mishipa, CCM imekuja na dhana mpya ya kujivua gamba iliyovuta hisia zenye ukinzani mkali wa hoja kutoka kwa wachambuzi tofauti wa masuala ya kisiasa.

Katika kuonyesha namna maradhi hayo yalivyokitafuna na yanavyoendelea kukidhoofisha chama hicho kwa kiwango cha kuwatia hofu viongozi wake, Rais Kikwete akaja na msamiati huo mpya.

Ili kuweza kujibu maswali ya wadadisi wa mambo wanaoisuta CCM wakisema inakabiliwa na tatizo kubwa la ombwe la uongozi, Kikwete akatumia mamlaka aliyopewa kuunda tume iliyojumuisha jopo la wataalam na wanazuoni wenye mapenzi mema na chama hicho.

Tume hiyo iliyojumuisha maprofesa na madaktari wa falsafa ikaongozwa na Wilson Mukama ambaye matokeo ya kazi waliyoifanya kwa muda wa wiki mbili kwa kujifungia katika hoteli moja kubwa ya nyota kadhaa yakamfanya ajikute akiukwaa ukatibu mkuu wa chama hicho.
Matukio haya yote ni kielelezo cha wazi kwamba, maradhi yale yale ya uongozi ambayo yamekuwa yakikitesa chama hicho kwa miaka nenda, miaka rudi yameendelea kukitafuna pasipo kukoma.

Pasipo kujua au pengine kwa mhemuko wa madaraka, Kikwete ambaye ndiye mwenyekiti wa taifa wa chama hicho akajitwika mzigo mzito wa kuongoza harakati za kukinusuru chama chake.
Huku akijua kuwa chama hicho kimelelewa katika misingi ya ‘zidumu fikra za mwenyekiti’ akajitwisha wajibu wa peke yake wa kuunda tume na kisha ili kuweza kukidhi utashi wake binafsi akajenga hoja ya kuwalazimisha wajumbe sekretarieti na wale wa kuchaguliwa wa kamati kuu kujiuzulu.

Yaliyofuata baada ya hapo sote tunayajua. Sekretarieti mpya ikaundwa huku nyuma na kwa siri ikibeba ajenda ya kuwalenga watu fulani fulani na wakati mwingine kupoza hasira za baadhi ya watu ambao angeweza kupata wakati mgumu kuwatupa kwa namna jongoo atupwavyo na mti wake.

Kinara katika sekretarieti mpya akawa Mukama, mtu ambaye tume yake ilibeba ajenda ya kuwashughulikia watu ambao tangu Kikwete aingie madarakani wamejikuta wakipita katika karai la moto kinyume kabisa na matarajio makubwa waliyokuwa nayo miaka sita tu iliyopita.

Kwa namna ile ile ilivyofanya kazi Kamati Teule ya Bunge iliyoongozwa na Dk. Harrison Mwakyembe miaka minne iliyopita, tume ya Mukama nayo ikawalenga watu wale wale na sababu zikiwa ni zile zile: Ufisadi.

Jasiri haachi asili. Kikwete yule yule aliyepata kuwanyoshea kidole ‘marafiki’ zake akisema kwamba urais wake hauna ubia, akakunjua makucha ya mamlaka safari hii akielekeza mashambulizi kwa kundi la watu wale wale ambao miaka kadhaa tu iliyopita walikuwa sambamba katika harakati za kusaka madaraka.

Baadhi yetu hatukupata shida kuelewa ni kitu gani kilikuwa kikitokea wakati tulipowasikia viongozi wapya wa CCM, Naibu Katibu Mkuu (Tanzania Bara), John Chiligati na Katibu wa Idara ya Uenezi na Itikadi, Nape Nnauye wakitangaza kile walichokiita Maazimio ya Halmashauri Kuu ya Taifa (NEC) ya CCM.

Taarifa ambazo zilivuja miongoni mwetu hata kabla ya kuanza kwa kikao hicho cha NEC, zilikuwa zikieleza bayana kwamba, wembe ulikuwa ni kuwang’oa fulani na fulani ndani ya CCM.

Hatukuwa na sababu ya kuuliza sababu za maamuzi hayo kuchukuliwa kwani sote tulijua fika kwamba, makusudi makubwa ya maamuzi hayo yalikuwa ni kinyang’anyiro cha urais cha mwaka 2015.

Watu tunaoufahamu utamaduni wa CCM wa kuhujumiana kisiasa na kulana wenyewe kwa wenyewe kama njia ya kupata madaraka katika taifa hili tukakumbushwa masahibu yaliyopata kuwakuta wanasiasa wa aina ya John Malecela, Frederick Sumaye, Dk. Salim Ahmed Salim na Iddi Simba wakati wa mchakato wa kuelekea Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2005.

Kwa sababu hiyo basi, tuliposikia walengwa wa safari hii wakiwa ni watatu tu, miongoni mwao wakiwa ni wale walioratibu ajenda za kuwamaliza wenzao mwaka 2005, tukaona tunao wajibu wa kuwaeleza wasomaji wetu kile ambacho kilikuwa kikiendelea ndani ya chama hicho tawala.

Wakati tukijifanya kidomodomo kuusema ukweli huo mchungu, tukasahau ukweli kwamba nyuma ya ajenda hii ya leo, wako vinara wawili ambao ndiyo waliokuwa wapishi wakuu wa majungu yaliyowamaliza akina Salim, Simba, Sumaye na Malecela.

Jambo baya zaidi, nyuma ya karata yetu hii ya kujifanya tukiwa vimbelembele kusimamia na kuutetea ukweli huu ulio bayana, tukajifanya tukiipuuza nguvu kubwa waliyonayo vinara wa mkakati huo ambao kinara wao ndiye mkuu wa kaya aliyeshika mpini wakati sisi tukiwa tumekamata makali.

Ukweli kwamba wapishi wa ajenda hii walikuwa na timu kubwa ya makachero walio serikalini na walio idarani ukawa silaha kubwa ya kutujeruhi, baadhi yetu vibaya sana.

Huku wakijua kwamba tulikuwa tumeshang’amua janja yao ya kutafunana wenyewe kwa wenyewe kwa gharama za kufifisha turufu muhimu ya ushindi wa demokrasia ya vyama vingi iliyoanza kuchanua katika uchaguzi mkuu uliopita, makachero hao wa CCM na mawakala wao walio serikalini, wakaja na uzushi ule wa siku zote.

Kwa ustadi mkubwa huku wakitumia uzoefu wao wa kupindisha mambo, makachero hao wakafanikiwa kupenya katika mioyo ya baadhi ya viongozi wa kidini na wale wa vyama vya siasa vya upinzani ambao wakajikuta wakishangilia dhana isiyo na mashiko ya CCM kujivua gamba.

Walipoona hilo halitoshi, wakarejea ndani ya vyumba vyetu vya habari na wakatumia udhaifu wetu wa kufikiri sawasawa kutulisha uzushi wao wakituaminisha kuwa ni wa kweli ukielekezwa kwanza miongoni mwetu na kisha miongoni mwa walengwa wakuu wa ajenda nzima ya kujivua gamba.

Ni jambo la bahati mbaya sana kwamba, makachero hao wamefanikiwa kwa kiwango kikubwa kulihadaa taifa kupitia vyombo vyetu vya habari na wakati mwingine kwa kuwatumia viongozi wa vyama vya siasa vya upinzani ambao hawajui kuwa ile dhana ya zidumu fikra sahihi za mwenyekiti (wa CCM) imeshapenya ndani ya mioyo yao.

Ni jambo la kukatisha sana tamaa kwamba, japokuwa sote kwa ujumla wetu tunatambua vyema kuwa ajenda nzima ya kujivua gamba iliyoasisiwa na mwenyekiti wa taifa wa CCM ina harufu ya dhuluma, uonevu, kupakana matope na kuua ustawi wa mfumo wa vyama vingi bado tumeendelea kushangilia maamuzi hayo.

Matokeo yake makosa yetu hayo yamesababisha wanahabari tujikute tukiwa mavuvuzela wa ajenda ya kujivua gamba, tukipaza sauti na kuimwagia sifa lukuki pasipo kujua kwamba tunafanya hivyo kwa gharama za ustawi wetu wenyewe wa sasa na wa siku zijazo.
Hitimisho la yote hayo linatufanya sote kama taifa, kwa kujua au kutojua tujikute tukiwa majeruhi wa dhana iliyopitwa na wakati ya zidumu fikra za mwenyekiti wa CCM pasipo kujali usahihi, malengo, makusudi na mwelekeo mzima wa kifalsafa wa fikra hizo. Hatupaswi kwenda huko.

photo

0 Responses so far.